Jumapili ya 16 ya Mwaka

 

Somo la Kwanza: Yer. 23:1-6

Wimbo wa katikati: Zab. 23, (K) 1,

Somo la Pilli: Waefeso. 2:13 -18

Injili: Mk. 6:30 - 34

Muhtasari wa Injili:

Nabii Yeremia alihudumu katika kipindi kigumu sana cha kisiasa katika historia ya watu wa Israeli. Viongozi wa kisiasa walikuwa mafisadi, waliopenda starehe badala ya kuangalia maslahi ya watu hasa watu wa kiwango cha chini kielimu na kiuchumi. Viongozi wa Israeli hawakuwa watu wa haki, waliwaachia watu wasio na hatia wadhulumiwe na mafisadi, waovu, wachochezi, na waeneza vurugu wabaki huru. Uzembe na kutojali kwa viongozi wa Israeli ulisababisha watu watu wengi wa Israeli kuchukuliwa utumwani Babeli. Nabii Yeremia akaripia uzembe na kutojali huko. Anatangaza utawala wa Masiya. Mitume katika Injili, wanarudi kutoa habari ya safari waliyotumwa kama tulivyosikia katika Injili ya Jumapili iliyopita, Yesu anataka waende faraghani sehemu isiyo na watu, wanatafakari juu ya kazi yao na wapumzike lakini muda huo wa kupumzika na kutafakari, unakatishwa na kundi kubwa la watu waliokua kama kondoo bila mchungaji.

Kondoo bila mchungaji:

Kondoo bila mchungaji ni kitoweo cha mbwa mwitu, simba na wanyama wakali. Katika enzi za Yesu, na kama zilivyo jamii za wachungaji kama wamasai siku za leo, uchungaji haukuwa kazi rahisi. Haku-ku-kuwa na ranches ambako mifugo walifungiwa salama. Mchungaji alitakiwa awe macho saa zote, usiku na mchana akihakisha kondoo wake wako salama kwani uzembe kidogo wa mchungaji ungegharimu maisha ya kondoo. Siku ya leo Yesu anawaona wana wa Israeli wakiwa kama kondoo bila mchungaji. Wachungaji wamezembea kazi yao, ama wanajiunga na kundi la wala kondoo na kondoo hawezi kutofautisha kati ya mbwa mwitu na mchungaji, kwani wote wanaleta madhara yaliyo sawa, kuharibu, kula na kutawanya kundi.

 

Masomo ya Jumapili ya leo yanatuonya tusiige mfano dhalimu wa viongozi dhalimu wanaoendekeza ulafi, ukabila, chuki, rushwa, ufisadi na mambo mengine yote yanayoleta mgawanyiko katika jamii. Ukiangalia nchi zetu hasa za Afrika na hasa chini ya jangwa la sahara tutakubali kuwa maneno aliyonena na nabii Yeremia miaka 2700 iliyopita bado ni ya kweli, viongozi wahuni, dhalimu, walafi na wanaonyang’ania madaraka bila kujali wananchi na maadili ya uongozi wanasababisha mateso mengi sana kwa wananchi wao. Tuchukue mfano wa Somalia, tuone jinsi ndugu zetu wa Somalia wanavyoteseka vita zaidi ya miaka 20 bila shughuli yoyote ya maendeleo, tuangalie DRC vita visivyo na kichwa wala mkia, mali asili waliyopewe na Mungu ili iwasaidie kuinua maisha yao, waishi kwa furaha imebadilishwa kuwa laana, vita vya kupigania kuiba madini na mali asili. Hizo ni nchi chache tu lakini hata nchi kama Tanzania, Kenya, Uganda bado watu wa maisha ya chini wananyanyasika vibaya sana kutokana na uzembe, ufisadi na kutojali kwa viongozi wa jamii na hata baadhi ya viongozi wa dini wamekubali kufadhiliwa na viongozi matajiri, mafisadi wasio jali masilahi ya watu. Tofauti na wakati wa Yesu ambapo hapakukua na democrasia ya kuchagua viongozi, siku hizi pamoja na kwamba democrasia haijakua bado unauwezo wa kufanya uamuzi sahihi. Unapokubali kununuliwa na viongozi ili uwapigie kura, ama unapomchagua kiongozi kwa sababu anatoka katika kabila lako ila siyo kwa ajili ya maadili na uwezo wake wa kuongoza bali na wewe una sehemu ya laana alivyolaani nabii Jeremia. Ni wajibu wako kama mkristo na mwananchi kuwaoea huruma watu wanaoteseka kutokana na viongozi wabovu, uwe nabii kwao na ushiriki mateso yao kwa njisi unavyoweza.

Sisi wote ni viongozi;

Masomo ya leo hayaongelei viongozi waliochanguliwa ama kujichagua kuongoza watu tu. Kila mtu ni kiongozi kwa nafasi yake. Ni kweli viongozi wanaongelewa na wale waovu wanalaaniwa lakini kila mmoja wetu ni kiongozi, ukiwa baba wa familia ni kiongozi na yafaa kuangalia ni jinsi gani unaepuka yale yote yaliyokemewa katika masomo ya leo katika familia yako na katika jamii yako kwa ujumla. Si viongozi pekee wanaotoa na kupokea rushwa. Siyo viongozi pekee wanaokuwa na maadili mabaya si viongozi pekee wanaoendeleza ulafi na mgawanyiko. Wewe kama baba, mama, ama mtoto umeendelezaje upendo, umoja na mtengamano katika familia? Je wewe umekuwa chanzo cha chuki liletacho mgawanyiko katika familia? Umekuwa ukichochea uonevu? Umekuwa chanzo cha ugomvi? Kutokana na tabia na mwenendo wa maisha unaoleta nsintofahamu katika familia? Je ukichukulia hiyo familia yako ndogo ya watu wanne ama saba uki-ikuza na kuwa nchi, wewe raisi, mke wako ama mume wako waziri mkuu na watoto na ndugu wabunge na mawaziri, unafikiri nchi hiyo yenu itakuwa na afadhali? Jibu unalo wewe na ukweli uko ndani ya moyo wako. Yesu katika Injili ya leo anatuonyesha mfano, pamoja na uchovu na kuujali uchovu wa wanafunzi wake, hakuweza kujizuia alivyouona umati mkubwa wa watu ukiwa kama kondoo bila mchungaji, wewe unapoona kondoo bila mchungaji na unashughuli nyingi umechoka unafanya nini?

Habari njema ni kwamba, Kristo anaujua udhaifu wetu wanadamu akamtuma Roho Mtakatifu kutupa nguvu ya kuamka tena na kuendelea tunapojikuta kumeangushwa na yale mambo yote yaliyo kinyume na ufalme wa Mungu.