Jumapili ya 11 ya Mwaka C
- Details
- Published on Saturday, 15 June 2013 05:58
- Written by Fr. Jude Mmassy OP
So mo la Kwanza: 2Sam. 12: 7 – 10, 13
Wimbo Wa Katikati: Zab. 31: 1-3-2,5,7,11,(K) 5
Somo La Pili: Gal. 2: 16, 19-21
Injili: Lk. 7: 36 – 8:3 ama 7:36-50
Utangulizi:
Mfalme Daudi alifanya mapenzi na Basheba mke wa Uria, askari mkuu wa jeshi la Daudi. Basheba anapata mimba, na Daudi anafanya mbinu ili Uria alale na mkewe ili kuificha dhambi ya Daudi. Mbinu zote za kumfanya Uria alale na mkewe Basheba zinashindikana kwa sababu Uria hawezi kufanya mapenzi na mkewe wakati vita inaendelea. Daudi akafanya hila na Uria akauawa na maadui katika vita. Tunachosikia katika somo la kwanza ni ujumbe wa Mungu kwa Daudi kupitia kinywa na nabii Nathani. Nathani anamkumbusha Daudi yale yote Mungu aliyomjalia lakini bado hakuridhika bali alikubali kutongozwa na tamaa za mwili. Daudi ameutoa uhai wa Uria na kutwaa mke wa Uria. Daudi amekubali dhambi yake na kutubu. Mungu anamuondolea adhabu ya kifo. Injili ya leo, ina sehemu mbili zisizo andamana. Sehemu ya kwanza ni karamu ya chakula nyumbani kwa Simoni, mfarisayo ambaye hakumpatia Yesu heshima ya ukaribisho aliyostahili. Mwanamke mwenye dhambi anajaziliza heshima iliyokuwa imeachwa na Simoni tena kwa ufanisi zaidi. Sehemu ya pili ni kundi la wanawake walioponywa na Yesu waliokuwa wakimhudumia Yesu na wanafunzi wake kwa mali zao.
Usisikie anayokuambia tu, angalia pia anavyokutenda
Ukitaka kujua anachoamini mtu usiya-amini tu maneno yake bali uangalie na maisha yake. Ukitaka kujua anayokuambia mtu juu yako ni kweli ama la, usiyasikie maneno yake tu bali mwangalie anavyokutenda. Maneno yasiyo ambatana na matendo ni ya uongo, ni ya kinafiki na ni ya kifarisayo. Simoni, mmoja wa Mafarisayo anamkaribisha Yesu katika chakula. Na mafarisayo walitofautiana kati yao, wengine waliamini kuwa Yesu ni nabii na wengine hawakuamini (rej. Yoh. 9:16). Simoni anamualika Yesu kama nabii lakini hamtendei yanayotakiwa nabii kutendewa.
Kwa desturi na utamaduni wa Wayahudi wakati wa Yesu, ukimualika rabi (mwalimu, nabii) nyumbani kwako kuna mambo matatu ambayo ungefanya:
- Ungeweka mikono yako mabegani kwake na kumbusu, kama ishara ya kumtakia amani nyumbani kwako.
- Wewe mwenyewe ama mjakazi wako angemuosha miguu
- Ungechoma ubani ama umdondoshee tone la marashi ya ua la waridi kichwani.
Simoni, pamoja na kumuita Yesu mwalimu na nabii hakufanya lolote kati ya yale aliyotakiwa kufanya. Maneno yake hayakuambatana na jinsi alivyomtenda Yesu. Alimpa Yesu huduma ya mdomo, alimuita mwalimu bila kumfanyia lolote ambalo alistahili kumtendea mwalimu. Mwanamke aliyekua na dhambi zilizojulikana anajaza pengo lililoachwa na Simoni.


